FROM ONE PERSONALITY TO ANOTHER
“Nakupenda sana, na natamani unielewe ila sijui ni maneno gani niyatumie.”
Siwezi kukadiria,
hasira nisiyojua,
kaka zako wanalia,
pale tu lijapo jua,
ni ngumu kufikiria,
pale watapoamua,
chuki yao ‘palilia,
haki yao kuchukua.
Uchungu huu wa mwana,
aujuae ni mzazi,
wamkwaza sana mama,
naomba ‘mtake radhi,
kwa kucheka na mabwana,
na kuacha zako kazi,
huwezi kwepa lawama,
kwa kujipandisha hadhi!
kila jicho juu yako,
wawezaje ‘pinga mila?
kusahau ndugu zako,
na kuzichochea hila,
funzo zote kuja kwako,
bado wakana kabila?
bila fimbo mbele yako,
unatoka bila bila.
Ninapenya ka’ mdudu,
hamuwezi kunidaba.
kutii na kusujudu,
hivi kwangu ni ibada,
nitabaki kuwa bubu,
niwapo kwenye minada,
dharau nitazimudu,
hata kutoka kwa baba.
Mimi msichana tu,
ni kipi naweza ‘fanya?
siwezi leta makuu,
nisije fanywa kibaya,
kabla ya kunihukumu,
na kisha kushika taya,
beba msalaba huu,
uonje machungu haya!
Japo sina cha kupenda,
kutoka kwa mabepari,
nazo chuki najitenga,
kuziepuka hatari,
hapo mabaya watenda,
walimishwa mahekari,
zikusanye chengachenga,
ungana na mahodari.
Ipo siku sitaweza,
kulea huu ujinga,
mtu mweusi kumbeza,
mweupe kuringaringa,
na mweupe kujikweza,
mweusi kumtingatinga,
siku hiyo ‘tawameza,
wachapa na kuwapinga.
“Kumbuka haya Mondala,
with a song from the cabin,
mateso ya fimbonyala, is more than you can imagine,
bila viatu au ndala, a towel or a napkin,
masaa matatu kulala, before the dogs start barking,
treated like a gorilla, what a life it has been,
Black Diamond you are and freedom is your calling.”